Waziri wa Utalii Rebecca Miano, ni miongoni mwa wajumbe wanaohudhuria Mkutano Mkuu wa 26 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Utalii nchini Saudi Arabia.
Mkutano huo unawaleta pamoja Mawaziri, maafisa wakuu wa serikali na viongozi wengine kusherehekea miongo mitano ya ushirikiano wa kimataifa kwa lengo la kupiga jeki sekta hiyo kupitia mazungumzo komavu.
“Leo najiunga na Mawaziri kuhusu athari za teknolojia na uvumbuzi katika kuimarisha sekta ya Utalii kwenye mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Utalii,” alisema waziri Miano kupitia ukurasa wake wa X.
Miano alisema mkutano huo ambao umejiri kwa wakati, ni muhimu sana ikizingatiwa mabadiliko ambayo yameshuhudiwa katika sekta hiyo.
Alisema kupitia wizara yake, serikali pia imewahusisha vijana katika mazungumzo hayo muhimu.
Mkutano huo umeandaliwa na wizara ya Utalii ya Saudi Arabia.