Rais Ruto: Serikali inawekeza katika miundombinu kuimarisha maisha ya Wakenya

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto amesema kuwa serikali inawekeza katika miundomsingi ambayo inaleta mabadiliko hapa nchini.

Kiongozi huyo wa taifa alidokeza kuwa ili kufanikisha ukuaji wa uchumi wa kijamii na pia kubuni fursa za kazi kwa wananchi, serikali inatekeleza miradi kama vile ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, masoko ya bidhaa za shambani na nyumba za malazi kwa wanafunzi.

Akizungumza Jumapili wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa soko la kisasa la Baragoi, kaunti ya Samburu, Ruto alisema lengo la serikali kutekeleza miradi hiyo, pia ni kuimarisha maisha ya wananchi.

Soko hilo ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi Milioni 190, utawasaidia wafanyabiashara 500 kupata mazingira bora ya kuendeleza biashara zao.

Wakati huo huo, Rais Ruto alitoa wito kwa Wakenya wanaomiliki bunduki kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa maafisa wa usalama, la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Rais alisema bunduki hizo zimesababisha vifo na uharibifu, akibainisha kuwa ni maafisa wa usalama, ndio tu walio na mamlaka ya kubeba Bunduki.

Share This Article