Mshukiwa wa mauaji ya Agnes Wanjiru akamatwa Uingereza

Tom Mathinji
2 Min Read
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Ingonga, amethibitisha kukamatwa kwa raia mmoja wa uingereza kuhusiana na kifo cha mkenya Agnes Wanjiru mwaka 2012.

Kulingana na Ingonga, mshukiwa huyo kwa sasa anazuiliwa na polisi nchini Uingereza na anatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama moja jijini London Novemba 14,2025 ili kusikizwa kwa ombi la kuachiliwa kwa dhamana kuhusiana na ombi la afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma  kwamba arejeshwe humu nchini.

Kwenye taarika kwa ukurasa wa X, mkurugenzi huyo alisema kikao cha kubainisha jinsi ya kushughulikia kesi hiyo kitaandaliwa Disemba 9,2025.

“Hatua hiyo muhimu inafuatia juhudi za pamoja zilizofanikishwa na maafisa wa Kenya na uingereza,” alisema Igonga kwenye taarifa hiyo.

Haya yamejiri majuma sita baada ya mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuanzisha mchakato rasmi ya kumtaka raia huyo arejeshwe nchini Kenya kuwajibikia kesi hiyo iliyodumu miaka 13.

Mnamo Septemba 16, 2025, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma alipata agizo la kukamatwa kwa mshukiwa huyo kutoka kwa mahakama moja ya Nairobi.

Na mnamo Oktoba 9,2025 mkurugenzi huyo alithibitisha kuwa stakabadhi zote zinazohitajika zilikuwa zimewasilishwa kwa afisi ya Mwanasheria Mkuu ili ziwasilishwe kwa mamlaka ya Uingereza.

Agnes Wanjiru, mama wa umri  wa miaka 21 aliyekuwa msusi wa nywele alitoweka Machi 31,2012 baada ya kuonekana mara ya mwisho katika hoteli ya Lions Court Lodge mjini Nanyuki.

Mwili wake baadaye ulipatikana kwenye tanki la maji taka kwenye hoteli hiyo hiyo Juni 5, 2012, hali iliyozua ghadhabu na shinikizo za kutekelezwa kwa haki.

Share This Article