ODM yalaani vurugu eneo bunge la Kasipul

Martin Mwanje
2 Min Read
Gladys Wanga - Mwenyekiti wa kitaifa wa ODM

Chama cha ODM kimelaani kukithiri kwa vurugu katika eneo bunge la Kasipul kuelekea uchaguzi mdogo uliopangwa kufanywa eneo hilo Novemba 27. 

ODM sasa ikitoa wito kwa asasi za usalama kuwachukulia hatua kali wanaohusika na vurugu hizo.

“Chama cha ODM kinalaani vikali vitendo vinavyoongezeka vya vurugu vinavyoshuhudiwa katika eneo bunge la Kasipul kuelekea uchaguzi mdogo wa Novemba 27,” alisema mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Gladys Wanga kwenye taarifa.

“Tunasikitika mno kutokana na ripoti kwamba mkutano wa amani uliowahusisha wapiga kura na uliofanywa na mgombea wetu Boyd Were ulivurugwa na wahuni wanaohusishwa na mgombea mmoja hiyo jana. Washambuliaji walivamia eneo la mkutano, kuharibu mali, na kuhatarisha maisha ya wakazi na kwa bahati mbaya kusababisha kupotea kwa maisha na kuwacha nyuma hofu miongoni mwa jamii,” iliongeza taarifa ya Wanga ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Homa Bay.

ODM ikizitaka asasi za usalama kuwachukulia hatua kali wapangaji na wafadhili wa vurugu hizo.

Aidha, IEBC imetakiwa kuhakikisha usawa kwa wagombea wote kuelekea uchaguzi huo.

Kiti cha eneo bunge la Kasipul kiliachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Ong’ondo Were.

Mwanawe marehemu mbunge huyo, Boyd Were, yuko mbioni kujaza pengo lililoachwa na baba yake.

Hata hivyo, anakumbana na ushindani mkali kutoka kwa wagombea wengine hususan mgombea huru Philip Aroko.

Share This Article