Rais William Ruto amesema Kenya imejitolea kuboresha na kupanua uhusiano wake na Marekani.
Akizungumza leo Ijumaa alipokutana na kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini Susan Burns katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa Kenya na Marekani zinafurahia ushirikiano thabiti unaochochea ukuaji katika sekta za biashara na uwekezaji, usalama, afya, teknolojia na elimu.
“Tumejitolea kuimarisha na kupanua ushirikiano huu kwa manufaa ya ustawi wa nchi hizi mbili,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa mazungumzo yao yaliangazia kuimarisha mipango ambayo inatekelezwa na nchi hizo mbili, pamoja na kutafuta fursa mpya za ushirikiano zinazoleta manufaa kwa raia wa mataifa hayo.