Wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) wamekubali pendekezo la Marekani la kukomesha vita nchini Sudan, ili kuruhusu kutolewa kwa misaada ya kibinadamu.
Kwenye taarifa, RSF ilisema imekubali kumaliza vita kwa misingi ya kibinadamu iliyopendekezwa na kundi la mpatanishi wa Quad linaloongozwa na Marekani, ambalo linajumuisha Saudi Arabia, Misri na milki ya Falme za Kiarabu, ili kushughulikia athari mbaya za kivita kwa binadamu na kuimarisha ulinzi wa raia.
Tangazo la RSF linajiri majuma mawili baada ya wanamgambo hao kuudhibiti mji mkuu wa Darfur Kaskazini,El Fasher.
RSF ilisema kwamba wana hamu ya kumaliza kabisa mzozo huo wa miaka miwili.
Hata hivyo, wanajeshi wa RSF wameshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki ya watu na unyanyasaji wa kingono.
Aidha, Jeshi la Sudan halijatoa maoni yoyote kuhusiana na swala hilo.
Mapema wiki hii, mshauri mkuu wa Marekani wa masuala ya Kiarabu na Afrika, Massad Boulos, alisema juhudi zinaendelea kuafikia makubaliano ya amani na kwamba pande zinazopigana zimekubaliana.