Ruto, Zelenskyy wajadili kuhusu Wakenya wanaozuiliwa Ukraine

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais William ruto na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika mkutano wa awali. Picha/Hisani.

Rais William Ruto na mwenzake wa Ukraine Volodymr Zelenskyy wameshiriki meza ya mazungumzo, swala kuu likiwa ni vijana wanaohadaiwa kushiriki vita kati ya Urusi na Ukraine.

Kupitia ukurasa wa X, kiongozi wa taifa alisema alimwomba Zelenskyy kufanikisha kuachiliwa huru kwa raia wa Kenya ambao huenda wanazuiliwa katika korokoro za Ukraine.

“Nilikuwa na mazungumzo ya kufana kwa njia ya simu na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, na tulijadili maswala kadhaa yanayohusu raia wa nchi hizi mbili,” alisema Rais Ruto.

Ruto alimshukuru Zelenskyy kwa kukubali wito wake, akisema wamekubaliana kuwahamasisha vijana dhidi ya kuhadaiwa kuingia katika vita hivyo hatari.

Kwa upande wake, Zelenskyy alimfahamisha Rais Ruto kuhusu uvamizi wa Urusi nchini mwake na kumshukuru kwa usaidizi wake.

Vile vile Zelensskyy alizungumzia uhusiano wa nchi hizi mbili akiahidi kuuboresha hata zaidi.

Aidha, alisikitikia uvamizi wa Urusi dhidi ya watoto wa Ukraine, akisema nchi yake itakashifu uvamizi huo kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa mwezi huu.

Share This Article