Vikundi 32 Isiolo vyaanzisha mfumo wa akiba kujilinda dhidi ya majanga

Martin Mwanje
3 Min Read

Takribani vikundi 32 vya wanawake na vijana katika Kaunti ya Isiolo vimeanzisha mpango wa kuweka akiba kwa pamoja ili kujilinda dhidi ya madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, kufuatia kuondoka kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ambayo awali yalikuwa yakitoa msaada wakati wa majanga kama vile ukame na mafuriko.

Kupitia mradi unaojulikana kama “Non Economic Loss and Damage” (NELD), unaotekelezwa na Shirika la Queen of Peace Initiative, wanachama wa vikundi vya akiba vijijini (VSLAs) kutoka jamii mbalimbali katika wadi za Ngaremara, Burat, Wabera na Bulapesa wamepatiwa mafunzo kuhusu umuhimu wa kupanga kwa ajili ya majanga ya siku za usoni, na kuachana na imani potovu hasa miongoni mwa jamii za wafugaji kwamba kupanga kwa ajili ya janga ni sawa na kulialika.

Akizungumza katika kijiji cha Daaba, wadi ya Ngaremara, wakati wa uzinduzi wa vifaa maalum vya akiba vya NELD, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Queen of Peace Initiative, Josphine Ekiru, alisisitiza kuwa majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi hayaepukiki, hivyo ni busara jamii kujitayarisha mapema ili ziweze kujisaidia hata kabla ya serikali au mashirika mengine kuingilia kati.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itawasaidia wanajamii kujiinua tena pindi wanapokumbwa na changamoto, hata iwapo msaada wa nje hautapatikana.

Mshauri wa kiufundi wa VSLAs, Hosea Kendagor, aliipongeza jamii ya Isiolo kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika kuokoa na kusimamia fedha tangu kuanzishwa kwa vikundi hivyo mwaka 2018.

Alibainisha kuwa baadhi ya vikundi vimekuwa vikigawana zaidi ya shilingi milioni moja kila mwaka, jambo linaloonyesha kuwa wana uwezo wa kutekeleza miradi inayofadhiliwa kupitia mifuko ya fedha za tabia nchi kama vile FLLOCA yaani (Financing Locally Led Climate Action Programme) na Carbon Funds.

Hata hivyo, Kendagor alilalamika kuwa katika mikutano ya kimataifa kuhusu tabia nchi (COP) kama ule unaotarajiwa kufanyika nchini Brazil wiki ijayo, sauti za watu wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi hazisikiki.

Aliwataka wadau kuhakikisha kunakuwepo na uwakilishi wa kweli wa jamii zilizoathirika.

Kila kikundi kati ya hivyo 32 vya wanawake na vijana kilipokea kifaa cha Non Economic Loss and Damage kwa ajili ya kuwekea akiba pamoja na mtaji wa kuanzia shilingi 25,000.

Share This Article