Wamiliki wa shule za kibinafsi pamoja na wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule hizo wameiomba serikali kuu kupitia Wizara ya Elimu kutoa mgao wa fedha kwa shule hizo.
Akizungumza wakati wa mahafali ya wanafunzi wa PP1 na PP2 katika shule za Highlands, kaunti ya Meru watakaojiunga na darasa la kwanza mwaka ujao, mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule za Kibinafsi kaunti ya Meru, Isaiah Baabu, alisema kuwa serikali inapaswa kutoa mgao wa fedha kwa shule za kibinafsi kwani wazazi wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Alisema kuwa wazazi wengi wanashindwa kulipa ada za shule kwa wakati, akiongeza kuwa wazazi wa shule za kibinafsi pia ni walipa kodi kama wale wa shule za umma.
Baabu pia aliiomba serikali kuu kupatia shule za kibinafsi wahudumu wa maabara za sayansi waliohitimu ili kuhakikisha usalama wa watoto na walimu.
Kauli hizo ziliungwa mkono na baadhi ya wazazi waliotoa wito kwa serikali kutoa mgao huo wa fedha.
Wazazi hao walisema watoto wote wanapaswa kutendewa kwa usawa bila kujali kama wanasoma shule za umma au za kibinafsi, kwani wote wanajiandaa kulitumikia taifa siku za usoni.
Wamiliki wa shule za kibinafsi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na ukosefu wa fedha, hali inayosababishwa na wazazi kushindwa kulipa ada kwa wakati, jambo ambalo limesababisha baadhi ya shule kufungwa.
Wakati wa mahafali hayo, wanafunzi walionesha vipaji vyao mbalimbali, jambo linaloendelezwa katika mtaala mpya wa elimu unaozingatia umilisi.