Rais wa zamani wa Ghana, viongozi wengine wamwomboleza Raila, Bondo

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais wa zamani wa Ghana Nana Akufo-Addo akiwa na viongozi wengine, alipotembelea kaburi la Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga huko Bondo

Wageni mbalimbali wanazidi kumiminika alikozikwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga huko Kang’o Ka Jaramogi, Bondo ili kutoa heshima zao kwa kiongozi huyo shupavu na wakati huohuo kuifariji familia ya marehemu. 

Raila, ambaye pia alikuwa kinara wa chama cha ODM, alifariki Oktoba 15 wakati akipokea matibabu nchini India.

Kumekuwa na pirikapirika nyingi nyumbani kwake huku viongozi mbalimbali wakimiminika hapo kuifariji familia ya “Baba” alivyojulikana Raila, tangu alipozikwa Oktoba 19.

Wa hivi karibuni kufika nyumbani hapo walikuwa viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, akiwemo Rais wa zamani wa Ghana Nana Akufo-Addo na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.

Mwenyekiti wa chama cha KANU Gideon Moi pia ni miongoni mwa waliofika nyumbani kwa Raila kuomboleza kifo chake na kuifariji familia.

“Nakosa sana kwa dhati mabadilishano yetu mazuri,” alisema Mudavadi wakati akikumbuka urafiki wao aliyosema ulivuka mipaka ya kisiasa.

Wote hao wakighubikwa na wingu la simanzi kufuatia kifo cha mwenda zake ambaye ametajwa na wengi kama kigogo wa kweli wa safari ya demokrasia nchini Kenya.

Wengine waliokuwepo ni pamoja na Mawaziri Wycliffe Oparanya wa Vyama vya Ushirika na Deborah Barasa wa Mazingira na Magavana wakiongozwa na Gavana wa Siaya James Orengo, miongoni mwa wengine.

Share This Article