Gavana Achani atoa pole kufuatia ajali ya ndege Kwale

Marion Bosire
2 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani.jpeg

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amedhihirisha huzuni kubwa kufuatia ajali mbaya ya ndege iliyosababisha vifo vya watu 12 katika wadi ya Tsimba Golini, kaunti ndogo ya Matuga, kaunti ya Kwale.

Kulingana na taarifa rasmi ndege hiyo iliyopata ajali ilikuwa imebeba watalii waliokuwa wakisafiri kutoka uwanja wa ndege wa Diani kuelekea hifadhi ya taifa ya wanyamapori ya Masai Mara katika kaunti ya Narok.

“Nimesikitishwa sana na ajali ya ndege iliyotokea Tsimba Golini, katika kaunti ndogo ya Matuga, Kwale, ambayo imesababisha vifo vya watu 12, wakiwemo watalii waliokuwa wakisafiri kutoka uwanja wa ndege wa Diani kuelekea hifadhi ya taifa ya Masai Mara,” alisema Gavana Achani katika ujumbe wake wa rambirambi.

Kwa niaba ya serikali ya kaunti na wananchi wa Kwale, Gavana Achani alitoa rambirambi za dhati kwa familia na marafiki wa walioangamia, akieleza ajali hiyo kuwa ni msiba mzito na wa kusikitisha.

Alizitaka familia zilizopoteza wapendwa wao kuwa na utulivu huku mamlaka husika zikiendelea kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Aidha, Gavana Achani aliwaonya madereva na watumiaji wa barabara katika kaunti hiyo kuwa waangalifu zaidi, kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha ambayo imesababisha watu kutoona barabara vizuri na kuleta hali hatarishi kwa madereva.

Serikali ya Kaunti ya Kwale inatarajiwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa kusaidia katika uchunguzi wa tukio hilo.

Share This Article