Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga ameondolewa kwenye wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, CoG.
Hatua hiyo imechukuliwa kwa kauli moja wakati wa mkutano usiokuwa wa kawaida wa baraza hilo ulioandaliwa leo Jumatano.
Nayo imetokana na hatua ya Kahiga kuonekana kudhihaki kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.
Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi amesema wataratibu mkutano mwingine baadaye wa kumchagua Naibu Mwenyekiti mpya wa baraza hilo.
Kahiga alinukuliwa kwenye video moja ambayo imesambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kusherehekea kifo cha Raila, wakati akihutubia hadhira katika eneo la Kieni jana Jumanne.
Kwenye video hiyo, Kahiga anasikika akisema eneo la Nyanza lilikuwa likifaidika sana na miradi ya maendeleo, lakini kwa sababu Raila amefariki, eneo la Mlima Kenya sasa litafaidika.
“Kama Baraza la Magavana, tungependa kujitenga kabisa na matamshi ya Gavana Kahiga na kuelezea kwamba hayo ni matamshi ya kibinafsi ambayo hayaakisi maoni ya Baraza la Magavana na hasa wakati huu wa maombolezo,” alisema mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatano.
“Tunaelezea kwamba matamshi hayo hakika ni ya kizembe, yasiyojali hisia za wengine, ya kuhuzunisha na kusikitisha. Ni ukosefu wa utu na haikubaliki kusherehekea kifo chake kwa misingi ya dhana ya miegemeo ya kisiasa. Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa, na daima atasalia kuwa kiongozi shupavu ambaye michango yake imeandikwa katika historia ya nchi yetu. Hakuwa tu mwanzilishi na baba wa Ugatuzi lakini mtetezi na mfuasi wake mkuu.”
Matamshi ya Kahiga yanajiri siku chache baada ya Raila aliyefariki Oktoba 15 kuzikwa nyumbani kwake huko Bondo Oktoba 19.
Viongozi wengi wa upinzani hasa kutoka Mlima Kenya hawakuhudhuria mazishi hayo.