Rais William Ruto ametuma ujumbe wa pongezi kwa Sanae Takaichi baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Japani.
Takaichi, mwenye umri wa miaka 64, anachukua mahali pa Shigeru Ishiba anayeondoka baada ya kujiuzulu wadhifa huo.
Yeye ni Waziri Mkuu wa 10 kuwahi kuhudumu kwenye wadhifa huo.
Aidha, yeye ni mwanamke wa kwanza kabisa katika historia ya nchi hiyo kuchaguliwa kama Waziri Mkuu.
“Ushindi wako ni ushuhuda wa imani iliyopo katika maono, uongozi na dhamira yako isiyoyumba kwa upigaji hatua na ustawi wa Japani,” alisema Rais Ruto kwenye ujumbe wake.
“Unapochukua usukani wa wadhifa huu unaostahili, ningependa kuthibitisha dhamira ya kudumu ya Kenya kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi zetu mbili.”
Ruto akiisifia Japani kwa mchango inaotoa kwa ustawi wa sekta mbalimbali nchini Kenya, msaada ambao anatumai utawala mpya utaendelea kuunga mkono.
Takaichi alijitosa siasani mara ya kwanza mnamo mwaka wa 2006 na amehudumu katika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwaziri kabla kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Japani.
Bunge la Japani leo Jumanne lilimchagua kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke kuwahi kuongoza nchi hiyo.
Hii ni baada ya kushinda kura zilizoandaliwa Oktoba 21.
Kuchaguliwa kwake kwenye wadhifa huo kumeidhinishwa rasmi na Mfalme Naruhito na hivyo kumfanya kushika rasmi hatamu za kuiongoza nchi hiyo.
Kiongozi huyo wa chama tawala cha Liberal Democratic, LDP anatarajiwa kuzindua serikali yake mpya ya muungano na Chama cha Japan Innovation, JIP.