Kenya, Senegal zaondoa vikwazo vya viza

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto akiwa na mwenzake wa Senegal Bassirou Diomaye Faye katika Ikulu ya Nairobi.
Raia wa Kenya na Senegal sasa wako huru kutembelea nchi hizo mbili bila kuhitajika kuwa na viza. 
Hii ni kufuatiwa kutiwa saini kwa makubaliano ya kuondoa vikwazo vya viza kwa raia wa nchi hizo mbili.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika leo Jumanne katika Ikulu ya Nairobi na kushuhudiwa na Marais William Ruto na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal.
Ruto alisema mpangilio wa kusafiri bila viza kwa kipindi cha hadi siku 90 utaimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Kenya na Senegal.
“Hatua hii kubwa itakuza uhusiano thabiti wa watu hadi watu na kuimarisha utalii, biashara na ushirikiano,” alisema Ruto.
Rais Faye yupo nchini kwa ziara rasmi na alikuwa mgeni mkuu wa sherehe za Siku ya Mashujaa zilizoandaliwa Oktoba 20 katika kaunti ya Kitui.
Viongozi hao wawili walitumia fursa hiyo kusisitiza dhamira yao ya pamoja ya kushirikiana kwa karibu katika nyanja za biashara, amani, nishati, michezo na masuala ya pande nyingi.
“Ushirikiano wetu katika nyanja hizi unalenga siyo tu kuboresha ustawi, lakini pia kukuza maendeleo endelevu kati ya nchi zetu,” aliongeza kiongozi wa nchi.
Kwa upande wake, Rais Faye alipongeza uhusiano kati ya Kenya na Senegal, akisema umejikita kwa amani, uthabiti, uongozi bora na utangamano wa Afrika.
Kuhusu biashara, Rais Faye alisema uhusiano wa pande mbili, biashara na uwekezaji hauakisi uwezo wake kamili, akiongeza kwamba mengi zaidi yanapaswa kufanywa kuangazia hili.
“Tumekubali kufanyia kazi kuratibu Tume ya Ushirikiano wa Pamoja, ambayo natumai itatambua na kutafuta nyanja madhubuti zinazohitaji kujengwa au kubuniwa,” alisema Faye.
Share This Article