Kaunti ya Kiambu imezuiwa kuwapiga kalamu madaktari wabobezi ambao ni wanachama wa Chama cha Madaktari nchini, KMPDU.
Jaji Hellen Wasilwa wa Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Wafanyakazi pia ametoa agizo la muda la kuzuia kaunti hiyo kuajiri madaktari wabobezi wapya.
Hii ni baada ya mwanasheria Henry Kurauka kuitaarifu mahakama kuwa madai ya kupigwa kalamu kwa madaktari hao na kuajiriwa kwa wengine yalikosa haki na kukiuka sheria za kazi na katiba.
Jaji Wasilwa ameiorodhesha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuitisha kikao cha kusikilizwa kwa kesi hiyo kitakacholeta pamoja pande zote husika.
Kikao hicho kitaandaliwa Oktoba 28.
Shughuli za matibabu katika kaunti ya Kiambu zimetatizika kwa kiwango kikubwa kufuatia mgomo wa wahudumu wa afya wanaoshinikiza kuangaziwa kwa maslahi yao ikiwa ni pamoja na malipo na mazingira bora ya kazi.
Hata hivyo, Gavana Kimani Wamatangi amekana madai ya kuwepo kwa mgomo huo akisema utoaji huduma za matibabu katika hospitali za umma unaendelea kama kawaida.
Amewalaumu mahasimu wake wa kisiasa kwa kubuni janga la afya lisilokuwepo.