Vijana wanaomezea mate kujiunga na idara ya polisi watajua ikiwa ndoto zao zitatimia mwishoni mwa mwezi huu.
Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Wafanyakazi kusikiliza pande husika kwenye kesi hiyo leo Jumanne.
Jaji Hellen Wasilwa amesema atatoa uamuzi juu ya kesi hiyo Oktoba 30 mwaka huu.
Kesi ya kupinga kusajiliwa kwa makurutu wapatao 10,000 wa polisi iliwasilishwa na aliyekuwa mbunge wa Kilome Harun Mwau.
Usajili wao, uliopaswa kufanywa kwa kipindi cha wiki moja, ulipaswa kuanza Oktoba 2 na kumalizika Oktoba 9.
Mwau akiwasilisha kesi dhidi ya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS inayoongozwa na Inspekta Mkuu wa Polisi na Tume ya Taifa ya Huduma za Polisi, NPSC.
Kwenye kesi hiyo aliyoiwasilisha chini ya cheti cha dharura, mbunge huyo wa zamani, miongoni mwa masuala mengine, anasema wajibu wa kusajili makurutu wa polisi unapaswa kuachiwa NPS wala siyo NPSC.
Pande hizo mbili zimekuwa zikivutana juu ya usimamizi wa malipo ya maafisa wa polisi huku kila upande ukidai kuwa na mamlaka ya kusimamia malipo hayo.
NPSC imeitaka mahakama kiutupilia mbali kesi ya Mwau ambayo imekwamisha shughuli ya usajili wa makurutu wa polisi.
Kulingana na tume hiyo, kesi hiyo inaibua masuala nyeti ya kikatiba na usalama wa taifa ambayo yapo nje ya himaya ya mahakama hiyo.