Kenya na Msumbiji zina uhusiano imara wa kidiplomasia uliodumu miaka 50. Hayo yamesemwa na Rais William Ruto.
Kiongozi wa taifa aliyasema hayo leo Jumanne, aliposhiriki meza ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Msumbiji katika Ikulu ya Nairobi.
Kulingana na Rais Ruto ushirikiano wa mataifa hayo mawili, umepigwa jeki na makubaliano katika sekta za Kilimo, Uchumi Samawati na uwekezaji.
“Mnamo mwezi Agosti mwaka 2023, nilifanya ziara ya kihistoria nchini Msumbiji, ambako tulitia saini mikataba minane ya maelewano. Mikataba hiyo ilijumuisha uongezaji dhamani kwa Majani Chai, Sukari na Kahawa,” alisema Rais Ruto.
Maswala mengine yaliyoangaziwa ni pamoja na ushirikiano katika uchumi wa baharini, usaidizi wa kisheria na utoaji mafunzo kwa Watumishi wa Umma.
Katika mazungumzo hayo, Rais Ruto aliishukuru makubaliano ya mwaka 2018, ya kuondoa hitaji la viza kwa raia wa nchi hizo mbili kwa siku 90, akisema hatua hiyo iliimarisha utangamano wa raia hao.