Wito umetolewa kwa jamii za kiafrika kuhamasisha wenzao zaidi kuhusu madhara ya ugonjwa wa polio na jinsi ya kuhakikisha ugonjwa huo unaondolewa kabisa katika ramani ya dunia.
Kwa mujibu wa Leonard Ithao, msimamizi wa Rotary Club, mataifa ya Afrika Mashariki ni kwamba japo kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa polio umeweza kudhibitiwa, ipo haja kubwa ya hamasa zaidi kutolewa kwa jamii ili kuhakikisha hakuna Mkenya au mwafrika anayeathirika tena na ugonjwa huo.
Wakiadhimisha wiki ya polio duniani katika eneo la Athi River kaunti ya Machakos, wameeleza kwamba jamii zinaweza kuanzisha kampeini za hamasa kupitia utamaduni wao jinsi zinavyoweza kujikinga na kuzuia kabisa uwepo wake.
Daniel Ngugi, mwathirika wa polio katika ujana wake, alielezea jinsi maisha yake yalivyobadilika kwa kiwango kikubwa na kulemaa kutokana na ugonjwa wa polio alipokuwa mdogo na hata kusababisha kupoteza marafiki.
Serikali kupitia Wizara ya Afya sasa imetakiwa kuweka mikakati mipya ya kuzuia uwepo wa polio nchini.