Rais William Ruto amesema kuwa serikali itajenga mabwawa 50 kote nchini, ili kupiga jeki utoshelevu wa chakula hapa nchini.
Akizungumza Jumatatu wakati wa sherehe ya Mashujaa katika kaunti ya Kitui, kiongozi wa taifa alisema kupitia mabwawa hayo, ekari milioni mbili za ardhi zitaweza kunyunyiziwa maji na kuimarisha uzalishaji wa chakula.
Kulingana na Rais Ruto, taifa hili hutumia kitita cha shilingi bilioni 500 kila mwaka, katika uagizaji chakula kutoka nje, zikiwemo mahindi, ngano, sukari na mafuta ya kupikia.
“Utegemeaji wa mvua kamwe hauwezi kukithi ongezeko la idadi ya watu inayoongezeka kila kuchao,” alisema Rais Ruto.
Rais alisema ni sharti taifa hili liweze kujitosheleza kwa chakula na hata kuweza kuuza nje ya nchi mazao kutoka hapa nchini katika miaka ijayo, huku akihimizz utumizi wa teknolojia ya kisasa katika sekta ya kilimo.
“Ni hitaji ambalo linapaswa kutimizwa kufikia mwongo ujao,” aliongeza kiongozi wa nchi.