ODM: Mwili wa Raila hautakesha nyumbani kwake Karen

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwili wa Raila Odinga hautakesha Karen.

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM), kimetangaza kuwa mwili wa Raila Odinga hautakesha nyumbani kwake Karen, lakini utapelekwa kwenye makafani ya Lee.

Kupitia kwa taarifa, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Philip Etale, hatua hiyo imetokana na sababu ambazo hazingeweza kuepukika.

“Baada ya shughuli ya umma ya kuutamaza mwili wa Raila katika uwanja wa taifa wa Nyayo, utapelekwa katika makafani ya Lee, kabla ya kusafirishwa Kisumu Jumamosi asubuhi,” alisema Etale.

Hapo awali, mwili wa Raila ulitarajiwa kukesha nyumbani kwake Karen, Jijini Nairobi, baada ya kukamilika kwa ibada ya mazishi katika uwanja wa Nyayo.

Hata hivyo kamati ya maandalizi ya mazishi ya Raila inayoongozwa kwa pamoja na Naibu Rais Kithure Kindiki na Seneta wa Siaya Oburu Odinga, ilibadilisha mpango huo ili kutoa fursa kutekelezwa kwa mchakato mzima wa uhifadhi wa mwili huo kabla ya mazishi.

Mwili wa Raila utasafirishwa Jumamosi asubuhi Jijini Kisumu, huku ibada ya ukumbusho itaandaliwa katiwa uwanja wa Kenyatta utakaohudhuriwa na Magavana, wabunge na wananchi wa eneo la Nyanza.

Share This Article