Madaktari waandamana Kiambu, Gavana Wamatangi asema sekta ya afya ni shwari

Martin Mwanje
2 Min Read
Wahudumu wa afya wakiandamana katika kaunti ya Kiambu Oktoba 13, 2025 / Picha kwa hisani ya mwanahabari wetu Ephantus Githua

Chama cha Madaktari nchini, KMPDU, leo Jumatatu kiliwaongoza wanachama wake kufanya maandamano kulalamikia kudorora kwa huduma za afya katika kaunti hiyo na kupuuzwa kwa matakwa yao. 

KMPDU inasema madaktari katika kaunti hiyo wamekuwa kwenye mgomo katika kipindi cha takriban miezi minne na nusu iliyopita, hali ambayo imelemaza huduma za matibabu kwa wakazi.

Wabunge kutoka kaunti ya Kiambu pia wamelalamikia kudorora kwa huduma za matibabu na kuutaka utawala wa Gavana Kimani Wamatangi kuchukua hatua madhubuti kuangazia tatizo hilo.

Hata hivyo, Gavana Wamatangi amepuuzilia mbali madai kwamba kuna janga la afya katika kaunti hiyo, akiyataja madai hayo kuwa porojo za kisiasa zinazoenezwa na mahasimu wake wa kisiasa.

Aliyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Thika Level 5.

Gavana Wamatangi akitaja madai hayo kuwa njama ya kisiasa inayokusudia kumchafulia jina.

Kulingana naye, huduma za matibabu katika hospitali za kaunti hiyo zinaendelea kama kawaida.

Ni kauli zilizoungwa mkono na kiongozi wa wengi Godfrey Mucheke na mwakilishi wadi ya Kamenu Peter Mburu walioandamana naye.

Wote hao wakiwatuhumu baadhi ya wanasiasa kutoka kaunti hiyo kwa kueneza porojo zinazokusudia kuwachochea wakazi kumchukia Gavana Wamatangi.

Hayo yanajiri siku chache baada ya hospitali ya rufaa ya Kenyatta, KNH kulalamikia idadi ya wagonjwa wanaofurika hospitalini hapo wakitafuta huduma za matibabu.

KNH imehusisha ongezeko la wagonjwa hao na mgomo wa wahudumu wa afya unaoendelea katika kaunti za Kiambu na Nairobi.

Share This Article