Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ameelezea imani kuwa mgombea wa chama tawala cha UDA katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Malava ataibuka mshindi wa uchaguzi huo utakaondaliwa Novemba 27.
Hii ni baada ya David Ndakwa kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kugombea wadhifa huo ulioachwa wazi kufuatia kifo cha Malulu Injendi mapema mwaka huu.
Ndakwa sasa atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Seth Panyako wa chama cha DAP-K na Edgar Busiega wa chama cha DCP.
DAP-K inashinikiza kuondolewa kwa Busiega kwenye kinyang’anyiro hicho ili kumpa mgombea wake fursa kubwa ya kuibuka mshindi.
“Nina imani katika wakazi wa Malava na nina imani kubwa kwamba mtatusaidia kupata kiongozi mzuri ambaye ni David Ndakwa,” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.
“Ndakwa, unapaswa kufanya kazi kwa karibu na viongozi wote kutoka eneo hili. Tafuta ndugu watakaokupa ushauri mwafaka, pata marafiki wengi zaidi na watu wazuri. Huu ndio ushauri wangu kwako.”
Mudavadi akiwaongoza wabunge sita kutoka eneo hilo kumuunga mkono Ndakwa kushinda uchaguzi huo mdogo.
Wabunge hao ni Fred Ikana (Shinyalu), Tindi Mwale (Butere), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Benard Shinali (Ikolomani), Nabii Nabwera (Lugari) na Titus Khamala (Lurambi).
Wote hao wameapa kufanya kampeni kali kuhakikisha mgombea huyo wa UDA anaibuka mshindi wa uchaguzi huo.
Uchaguzi mdogo wa Malava unachukuliwa kama kipimajoto cha ubabe wa kisiasa kati ya utawala wa Kenya Kwanza na upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale, kutoka UDA, ametofautiana na chama hicho na anamuunga mkono Panyako kutwaa uongozi wa eneo hilo.