EACC yakusanya shilingi Milioni 69 baada ya kunadi mali ya Obado na Osiro

Tom Mathinji
1 Min Read
EACC yanadi mali ya Obado na Osiro Jijini Nairobi.

Tume ya Maadili na kupambana na ufisadi EACC, imenadi mali ya thamani ya mamilioni ya pesa iliyomilikiwa na aliyekuwa gavana wa Migori Okoth Obado,  na aliyekuwa msimamizi wa hazina ya kaunti ya Nairobi Stephen Ogaga Osiro.

Kupitia taarifa kwenye ukurasa wa X, EACC ilisema mali hiyo iliuzwa Alhamisi Oktoba 9,2025 Jijini Nairobi ambayo ilikuwa ni pamoja na nyumba ya vyumba vitatu vya malazi mtaa wa Riara yenye thamani ya shilingi milioni 14, nyumba mbili katika mtaa wa Greenspan zenye thamani ya shilingi milioni 6.7 na nyingine milioni 11, na nyumba moja katika mtaa wa Loresho Ridge yenye thamani ya shilingi milioni 31.

Kulingana na tume hiyo, shilingi 69,705,000 zilikusanywa kutokana na uuzaji wa mali hiyo, na kwamba fedha hizo zitawekwa kwenye Hazina Kuu ya Taifa.

Tume hiyo imesema nyumba zote ziliuzwa kwa bei ya juu kuliko ilivyokadiriwa.

EACC awali ililenga kurejesha shilingi bilioni 1.9 zinazodaiwa kuporwa na Obado na washirika wengine 20 kutoka serikali ya kaunti ya Migori, kupitia kandarasi ghushi za ununuzi.

Obado na EACC hata hivyo waliafikiana kutwaliwa kwa mali yenye thamani ya shilingi milioni 428.

Share This Article