Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi nchini, KNUN Seth Panyako yuko huru kugombea ubunge katika eneo bunge la Malava katika uchaguzi mdogo utakaondaliwa katika maeneo 24 nchini Novemba 27.
Hii ni baada ya Panyako kupata idhini ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kugmbea wadhifa huo kwa tiketi ya chama cha DAP-K, hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wafuasi wake.
Awali, kulikuwa na uvumi kwamba Panyako angezuiwa kugombea wadhifa huo kwani alikawia kujiuzulu wadhifa wa serikali kwa wakati mwafaka kama inavyotakikana kisheria.

Seneta wa Kakamega Dkt. Boni Khalwale (kutoka chama cha UDA) aliyeandamana na kinara wa DAP-K Eugene Wamalwa, aliwaongoza wafuasi wa Panyako kusherehekea hatua yake ya kuruka kiunzi cha kwanza kuelekea bunge.
Kiunzi cha pili kinasalia kuwa mgombea wa chama wa chama tawala cha UDA David Ndakwa ambaye pia anaungwa mkono na chama cha ODM.
Khalwale na Wamalwa wakielezea imani kwamba Panyako ataibuka kidedea kwenye uchaguzi huo ambao unatarajiwa kutumiwa kama kipima joto cha ubabe kati ya serikali jumuishi na upande wa upinzani.
Aidha, Gavana George Natembeya wa Trans Nzoia na mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya ni miongoni mwa wanaomshabikia Panyako.

Kwa upande mwingine, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa wanatarajiwa kuongoza kampeni kali za kumpigia debe Ndakwa kuchaguliwa mbunge mpya wa Malava.
Panyako na Ndakwa nao wako mbioni kurithi kiti kilichowachwa wazi na Malulu Injendi aliyefariki mapema mwaka huu.