Wahadhiri wasimama kidete, wasema hawaterejea kazini hadi walipwe

Mgomo wa wahadhiri ulianza Septemba 17 na umelemaza masomo katika vyuo vikuu vya umma kwa kipindi cha wiki tatu sasa. Wanasema watarejea tu darasani baada ya matakwa yao kutimizwa kikamilifu.

Martin Mwanje
2 Min Read

Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma nchini waliandamana leo Jumatano jijini Nairobi kushinikiza serikali kuwalipa malimbikizi ya mshahara wao wanaosema yamefikia kima cha shilingi bilioni 7 kufikia sasa.

 Kima hicho kinakinzana na kile cha serikali inayosema inadaiwa shilingi milioni 600 na wahadhiri hao.

Wakiongozwa na Makatibu Wakuu Dkt. Constantine Wasonga wa UASU na Dkt. Charles Mukhwaya wa KUSU, wahadhiri hao wametaja kama dhihaka kima cha shilingi bilioni 3 zilizotolewa na serikali kama malipo yao.

“Huwezi ukatupa mzaha wa mwaka! Shilingi bilioni 3 katika kipindi cha miaka minne kwa vyama vyote?” alishangaa Dkt. Wasonga wakati akiwahutubia wanahabari.

“Kumaanisha shilingi bilioni moja kwa UASU, nyingine kwa KUSU na shilingi bilioni moja kwa KUDHEIHA? Tuvumilie wanafunzi wetu. Tunaisafisha sekta ya elimu ya juu ambayo imetelekezwa kwa miaka mingi iliyopita.”

Dkt. Wasonga akirejelea mgomo wa UASU wa mwaka 2003 aliosema ulidumu kipindi cha miezi tisa lakini mwishowe ukazaa matunda.

“Tunaenda kuwa na mgomo mrefu. Tunawapenda wanafunzi wetu, lakini tunalizimishwa kuwa nje,” aliongeza Katibu Mkuu huyo wa UASU aliyeapa kwamba kamwe hawatarejea darasani hadi matakwa yao yatimizwe kikamilifu.

Wahadhiri wakiinyoshea Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kidole cha lawama kwa kuwa kikwazo kwa juhudi za kusuluhisha mvutano kati yao na serikali.

Kulingana nao, SRC imejitwika jukumu la kuamua mishahara yao badala ya kutoa ushauri.

“Tunapaswa kushiriki mazungumzo na mwajiri wetu wala si SRC. Ikiwa SRC iko radhi kushiriki mazungumzo nasi, basi waje tufanye mazungumzo,” alisema Dkt. Wasonga aliyeonekana kupandwa na mori si haba.

Mgomo wa wahadhiri wa vyuo vikuu ulianza Septemba 17 na umelemaza masomo katika vyuo vikuu vya umma kwa kipindi cha wiki tatu sasa.

Wakati pande hizo mbili zikivutana, wanafunzi wanaendelea kuathirika kimasomo wakati mgomo huo ukikosa kuonyesha abadan dalili yoyote ya kufikia kikomo.

Share This Article