Serikali inakadiria uwezekano wa kuwajumuisha viongozi wa wanafunzi na Maafisa wa Usalama katika Vyuo Vikuu kwenye kamati za usalama za kaunti na kaunti ndogo, kuhakikisha changamoto za wanafunzi zinashughulikiwa mapema.
Katibu katika wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kuimarisha kuwahusisha vijana kwenye mfumo wa usalama na kufanikisha usalama katika taasisi za masomo.
“Lazima tuwakumbatie viongozi wa wanafunzi katika mifumo hii, ili tuweze kukusanya habari kwa wakati na kusuluhisha changamoto mapema,” alisema Dkt. Omollo.
Katibu huyo alitoa wito kwa taasisi za elimu kushirikiana kwa karibu na kituo cha kitaifa cha kukabiliana na ugaidi (NCTC), ili kuwezesha majadiliano kuhusu itikadi kali.
“Lengo letu ni kuhakikisha mazingira salama ya masomo. Usalama huanza kwa uhamasishaji, ushirikiano na uwajibikaji,” aliongeza Omollo.
Dkt. Omollo aliyasema hayo alipoongoza mkutano wa Jukwaa La Wasomi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Miongoni mwa maswala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na utumizi wa mihadarati, ukosefu wa usalama katika Vyuo Vikuu, dhuluma za kijinsia, itikadi kali, Afya ya Akili, Maadili na ukosefu wa ajira.
Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa vijana katika Vyuo Vikuu, wasimamizi wa vyuo vikuu na wawakilishi kutoka taasisi za elimu ya juu.