Waisraeli walikusanyika nchini kote kuadhimisha miaka miwili tangu shambulio lililoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, huku mazungumzo yakiendelea nchini Misri kuhusu kumalizika kwa vita huko Gaza.
Shambulizi hilo lilishuhudia zaidi ya watu 1,200 wakiuawa na wengine 251 kurudishwa Gaza kama mateka. Ilikuwa siku moja mbaya zaidi kwa Wayahudi tangu mauaji ya Holocaust.
Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi huko Gaza ambayo yameua zaidi ya watu 67,000, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Takwimu zake zinaonekana kuwa za kuaminika na UN na mashirika mengine ya kimataifa.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa yake kwamba pamoja na “maumivu makubwa”, Israel imeonesha “ustahimilivu wa kimiujiza”.
Wakati huo huo, timu za mazungumzo za Israel na Hamas zilikutana katika eneo la mapumziko la Bahari ya Shamu la Misri la Sharm el-Sheikh kwa siku ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kujadili masharti ya pendekezo hilo.
Afisa mkuu wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC kwamba kikao cha asubuhi kilimalizika bila matokeo yanayoonekana, huku kukiwa na kutoelewana kuhusu mapendekezo ya ramani ya Israel ya kujiondoa kutoka Gaza na juu ya dhamana ya Hamas inataka kuhakikisha Israel haianzishi tena mapigano baada ya awamu ya kwanza ya mpango huo.
Aliongeza kuwa mazungumzo hayo ni “magumu na bado hayajaleta mafanikio yoyote ya kweli,” lakini alibainisha kuwa wapatanishi wanafanya kazi kwa bidii ili kupunguza mapengo kati ya pande hizo mbili.
Hapo awali, afisa wa Palestina alisema mazungumzo hayo yalilenga katika masuala matano muhimu: usitishaji vita wa kudumu; kubadilishana mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas kwa wafungwa wa Kipalestina na wafungwa kutoka Gaza; kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka Gaza; mipango ya utoaji wa misaada ya kibinadamu; na utawala wa baada ya vita wa eneo hilo.