Makatibu wa wizara mbalimbali leo Jumatatu walitua katika kaunti zao za nyumbani ili kuandaa makongamano ya uhamasishaji wa mpango wa kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana humu nchini, unaofahamika kama Nyota.
Makatibu hao walihamasisha wadau kuhusu mpango huo utakaogharimu kima cha shilingi bilioni 5 kufuatia agizo la Rais William Ruto.
Hususan, mpango unadhamiria kuwawezesha vijana wapatao 100,000 kwa kuwapa mtaji wa kuanzisha biashara, kunoa ujuzi wao na kuwapa mafunzo ya kufanikiwa katika ujasiriamali.
Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni alitembelea kaunti yake ya nyumbani ya Kirinyaga kwa uhamasishaji wa mpango huo wakati mwenzake katika Wizara ya Usalama wa Taifa akizuru kaunti ya Homa Bay.

Katibu katika Idara ya Huduma za Watoto Carren Ageng’o alihamasisha mpango wa Nyota katika kaunti yake ya nyumbani ya Kisumu huku mwenzake katika Wizara ya Mazingira Festus Ngeno akifanya hivyo katika kaunti ya Nakuru.
Katibu wa Vyuo vya Kiufundi, TVET Esther Muoria aliandaa kongamano la uhamasishaji wa mpango huo katika kaunti ya Embu.
Hali ilikuwa vivyo hivyo kwa makatibu wengi serikalini walioandaa makongamano ya kuwahamasisha wadau mbalimbali kuhusiana na mpango huo.