Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA nchini Tanzania kimesema kwamba mwenyekiti wake Tundu Lissu yuko tayari kabisa kwa shughuli ya kusikilizwa kwa kesi inayomkabili ya uhaini.
Haya yanajiri wakati ambapo kesi hiyo inaanza kusikilizwa mfululizo leo Oktoba 6, 2025.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, alitoa taarifa jana Jumapili Oktoba 5, 2025 akielezea kwamba Lissu yuko tayari na maandalizi yote yamekamilika.
Taarifa ya Rupia ilielezea kwamba upande wa Jamhuri ndio utaanza kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama ukitarajiwa kuwasilisha mashahidi 30 huku vielelezo 11 vikiwasilishwa rasmi mbele ya Jaji.
CHADEMA imewataka Watanzania kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hiyo huku wakitoa wito wa mshikamano wa kitaifa.
“Tunaomba Watanzania wote waendelee kusimama na Mwenyekiti wetu katika kudai haki, ukweli na kulinda misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.” ilisema taarifa hiyo ya CHADEMA.
Kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, inatarajiwa kusikilizwa mfululizo mahakamani Oktoba 6 hadi Oktoba 24 2025 na kuendelea tena Novemba 3 hadi 12 2025.
Ratiba hii inaonekana kuthibitisha kwamba kweli Lissu hatoshiriki uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaoandaliwa Oktoba 29, 2025 ambapo alitarajiwa kuwania Urais.
Kesi hii imevutia hisia za wengi ndani na nje ya Tanzania, ikihusisha masuala nyeti ya kisiasa na haki za kiraia. Watetezi wa haki za binadamu na wadau wa demokrasia wanatarajiwa kufuatilia kwa ukaribu mwenendo mzima wa kesi hiyo.