Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimekanusha vikali madai yanayosambaa kuhusu hali ya afya ya kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga.
Katika taarifa ya leo Oktoba 5, 2025, iliyotiwa saini na Dennis Onyango, Chama hicho kimetaja uvumi huo kuwa upotoshaji wa kimakusudi unaoenezwa na wapinzani wa kisiasa wanaotafuta umaarufu.
ODM imekosoa vikali kundi linaloongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa, ikiwatuhumu kupanga njama ya kuaminisha umma kwamba Odinga ni mgonjwa.
Chama hicho kilihusisha kampeni hiyo na jaribio la kupunguza ushawishi wa kisiasa wa Odinga, likikumbuka kuhusu mashambulizi ya aina hiyo wakati wa azma yake ya kugombea Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mapema mwaka huu.
“Tumeona jinsi walivyoshirikiana na vyombo vya habari vya kawaida ambavyo sasa vinatangaza taarifa kutoka kwa wanablogu wasioaminika, hata kutumia picha bandia zilizotengenezwa na akili mnemba” ilisema taarifa hiyo.
ODM inasisitiza kwamba Odinga amekuwa wazi kuhusu hali yake ya kiafya na “Hajawahi kuficha hali yake—iwe ni mwaka 2010 alipokuwa Waziri Mkuu au 2021 alipogunduliwa na Covid-19”.
Kwa mujibu wa ODM, Raila alisafiri nje ya nchi Ijumaa, safari ya kibinafsi, moja kati ya nyingi alizofanya mwaka huu. Chama kimekanusha madai kwamba alielekea barani Ulaya na kuthibitisha kuwa hana matatizo ya kiafya.
“Raila bado yuko imara na amejitolea kwa dhati kwa misingi ya Serikali Jumuishi,” ODM ilisisitiza, ikitaja uvumi huo kama “ndoto za mchana” za wapinzani waliokata tamaa kwa kuona ushawishi wa Raila ukiendelea kudumu.