Trump aidhinisha kupelekwa kwa kikosi cha ulinzi kitaifa Chicago

Marion Bosire
3 Min Read

Rais wa Marekani Donald Trump ameidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi 300 wa Kikosi cha Ulinzi cha Kitaifa mjini Chicago, akitoa amri hiyo baada ya wiki kadhaa za vitisho licha ya pingamizi kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.

Jaji mmoja huko Oregon alikuwa amesitisha kwa muda mpango wa utawala wa Trump wa kupeleka Kikosi hicho cha Ulinzi cha Kitaifa katika jiji la Portland.

“Rais Trump ameidhinisha wanajeshi 300 wa Kikosi cha Kitaifa kuwalinda maafisa wa serikali ya shirikisho na mali zake” alisema msemaji wa Ikulu, Abigail Jackson Jumamosi.

“Rais Trump hatapuuza uhalifu unaoendelea kuikumba miji ya Marekani.” Aliongeza Jackson.

Gavana wa Illinois wa chama cha Democratic, JB Pritzker, alitangaza mpango wa Trump mapema Jumamosi baada ya maafisa wa Ulinzi wa Mpaka wa Marekani kumpiga risasi mwanamke mwenye silaha huko Chicago.

Msemaji wa Idara ya Usalama wa Ndani alisema katika taarifa kuwa hakuna afisa wa usalama aliyejeruhiwa vibaya katika tukio hilo ambapo kundi lililojumuisha mwanamke huyo aliyepigwa risasi liligonga magari ya Shirika la Uhamiaji na Forodha (ICE) kwa magari yao.

Mwanamke huyo, ambaye ni raia wa Marekani na ambaye jina lake halikutajwa, alijipeleka mwenyewe hospitalini, kulingana na taarifa hiyo.

Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusu hali yake kwa wakati huo. Maafisa wa ICE walitumia pilipili ya machozi na risasi za mpira katika makabiliano makali na waandamanaji siku ya Jumamosi.

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem, alisema kupitia chapisho kwenye X kuwa alikuwa anatuma vikosi maalum vya operesheni kudhibiti hali katika mtaa wa Brighton Park, Chicago.

Shirika la Uhamiaji na Forodha (ICE) limeanzisha operesheni mjini Chicago kuwalenga wahamiaji wasio na vibali waliotenda uhalifu, licha ya kupingwa na Gavana wa Illinois, JB Pritzker, na Meya wa Chicago, Brandon Johnson.

Pritzker alisema Kikosi cha Ulinzi kilipokea taarifa kutoka Pentagon asubuhi hiyo kuwa wanajeshi wangetumwa. Hakuweka wazi ni lini au wapi watapelekwa, lakini Trump amekuwa akitoa vitisho vya muda mrefu vya kupeleka wanajeshi Chicago.

“Asubuhi ya leo, Idara ya Vita ya Utawala wa Trump ilinipa onyo: peleka wanajeshi wako, au sisi tutafanya hivyo,” alisema Pritzker katika taarifa. “Hili ni jambo la kushtua na kinyume kabisa na maadili ya Marekani kudai kwamba Gavana apeleke wanajeshi wa kijeshi ndani ya mipaka yetu wenyewe bila ridhaa yetu.”

Msemaji wa ofisi ya gavana alisema hangeweza kutoa maelezo zaidi. Ikulu na Pentagon hawakujibu maswali kuhusu kauli ya Pritzker.

Share This Article