Mahakama Kuu imeamua kwamba Wakili na aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria nchini Kenya – LSK, Nelson Andayi Havi, anawajibika kulipa madeni ya ushuru ya kipindi cha Januari 2015 hadi Oktoba 2023.
Uamuzi huo umetokana na mzozo wa muda mrefu kati ya kampuni ya wakili huyo, Havi & Company Advocates na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya -KRA, ambayo ilitoa tathmini za ziada za ushuru na kukataa kumpatia cheti cha uzingatiaji ushuru kwa misingi ya ushuru wa mapato na VAT ambao haukulipwa.
Havi alipinga tathmini hizo mbele ya jopo la kutatua mizozo ya ushuru, akidai kuwa hatua za KRA zilikuwa zimepitwa na muda na zilikuwa kinyume cha sheria.
Hata hivyo jopo hilo liliamua mwezi Januari 2025 kwamba pingamizi za Havi ziliwasilishwa nje ya muda wa kisheria na hivyo kuwa batili na likatupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa mamlaka.
Havi alikata rufaa katika Mahakama Kuu, ambayo ilitambua kuwa rufaa yake ilikuwa halali lakini ikaunga mkono msimamo wa KRA.
Mahakama ilibaini kuwa pingamizi la kuchelewa alilowasilisha mwezi Julai 2022 halikukubalika kisheria licha ya kupatiwa muda wa nyongeza.
Mahakama ilihitimisha kuwa tathmini na notisi za madai kutoka KRA zilikuwa halali, na kwamba madeni ya ushuru lazima yalipwe. Hukumu hiyo imesisitiza umuhimu wa kuzingatia muda wa kisheria chini ya Sheria ya Taratibu za Ushuru.