Kamati ya Bunge la kitaifa kuhusu uhusiano wa kikanda imeahidi kuharakisha kuridhiwa kwa marekebisho muhimu ya itifaki ya umoja wa forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC.
Hatua hiyo itawezesha nchi zaidi kujiunga na kamati ya kusuluhisha migogoro ya biashara ya jumuiya ya EAC.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Irene Mayaka, alithibitisha mpango huo katika kikao na maafisa wa idara ya jumuiya ya Afrika mashariki akisema, “Kamati hii itahakikisha Bunge linapitisha kuridhiwa kwa marekebisho ya Kifungu cha 24(2) cha Itifaki.”
Kwa sasa, ni Kenya, Uganda na Tanzania pekee ndizo zinawakilishwa kwenye Kamati hiyo.
Marekebisho yaliyopendekezwa yataruhusu Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia kuteua wanachama na hivyo kupanua ushirikiano wa kanda katika kutatua migogoro ya kibiashara.
Katibu wa uhusiano wa kikaanda Alice Yalla, alisisitiza kuwa marekebisho hayo, yaliyowasilishwa kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 2017, yamecheleweshwa sana.
Alihakikishia Kamati kuwa kuridhiwa kwake kutaimarisha nafasi ya Kenya kibiashara na kuongeza uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni.
“Kenya tayari ni mnufaika mkubwa zaidi katika eneo hili,” alisema Yalla. “Kuridhiwa huku kutaimarisha zaidi mafanikio yetu.” Aliongeza.
Hata hivyo, Kamati ilieleza wasiwasi kuhusu masuala kama mvutano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania na kuchelewa kwa baadhi ya nchi wanachama wa EAC kutekeleza majukumu yao ya kifedha.
Yalla alisema mazungumzo ya kidiplomasia yanaendelea na Idara yake imejitolea kupata suluhisho la haki na kwa wakati.
Mara tu marekebisho yatakaporidhiwa, nchi zote wanachama wa EAC zitaweza kutekeleza kanuni za asili ya bidhaa, kudhibiti hatua za ulinzi wa biashara na kukuza biashara ya haki kikanda.