Wizara ya ulinzi yaitwa bunge kisa mwanajeshi aliyefutwa

Marion Bosire
2 Min Read
Tonny Soya Muok

Wizara ya ulinzi ya Kenya imetakiwa kufika mbele ya kamati ya bunge kuhusu ulinzi, ujasusi na masuala ya ughaibuni, baada ya kunyoshewa kidole cha lawama na mwanajeshi wa zamani anayedai kufutwa visivyo na kudhulumiwa.

Jamaa huyo kwa jina Tonny Soya Muok alifika mbele ya kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Nelson Koech ambapo alidai kwamba alikuwa amelazwa katika hospitali ya wanajeshi, kipindi anachodaiwa kutelekeza kazi.

Usimamizi wa jeshi hilo la la KDF hata hivyo unashikilia kwamba Tony alikosa kufika kazini kwa takribani siku 19 na hakuwa amepatiwa likizo rasmi.

Jamaa huyo aliyekuwa mwanamaji anajitetea akisema kwamba wakubwa wake kazini walikuwa wanafahamu kwamba alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na jeraha ambalo hakulitaja lakini wakaamua kuripoti kwamba alitelekeza kazi.

Tony aliyejiunga na jeshi mwaka 2008 anasema anadaiwa shilingi milioni 1.5 na KDF.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Bashir Abdullahi alitaja Sheria ya KDF ya mwaka 2012 inayosema kuwa afisa wa KDF anaweza kurejeshwa kazini tu baada ya kukaa nje ya jeshi kwa kipindi cha miaka mitatu na kupitia mapitio ya mafanikio kuhusu kufutwa kwake kazi.

Tony hata hivyo amekaa nje ya jeshi la wanamaji kwa miaka saba tangu alipotimuliwa mwaka 2018 ambapo Bashir, ambaye ni meja mstaafu, alimshauri Tony aombe fidia kwa kufutwa kazi kimakosa lakini aache wito wa kurejeshwa kazini.

Tony alisema tangu afutwe kazi, aliripoti suala hilo kwa Tume ya Haki za Utawala (CAJ) ambayo iliandika barua kwa KDF kwa niaba yake, lakini tangu wakati huo suala lake halijawahi kusikilizwa na Kitengo cha Nidhamu cha Jeshi.

Mwenyekiti wa kamati, Koech, alisema kuwa kamati inayoongozwa na Soipan Tuya itafika mbele yao na kujibu tuhuma zilizotolewa na afisa huyo wa zamani wa KDF.

Share This Article