Mtayarishaji wa muziki maarufu nchini Tanzania Salmin Kasimu Maengo maarufu kama S2kizzy au ukipenda Zombie, amemshukuru mwanamuziki Diamond Platnumz kwa kutoa msaada wa fedha kwa mtayarishaji muziki aitwaye Bacteria mwenye makao yake huko Tanga.
Haya yanajiri wiki moja tu baada ya S2kizzy kuangazia suala la Bacteria kwenye mitandao ya kijamii ambapo alimzuru akampa usaidizi na kuhimiza wengine pia kutoa mchango wao.
Bacteria alipooza miguu kufuatia majeraha aliyopata yapata miaka miwili iliyopita katika kisa cha kuvamiwa na wahuni alipokuwa akitoka kazini usiku.
Leo S2Kizzy amechapisha video ambapo anashuru Platnumz kwa mchango wa Dola elfu 15, pesa taslimu ambao alitoa kwa Bacteria kupitia kwa S2kizzy.
Diamond alijibu ujumbe aliochapisha S2kizzy akisema, “Hongera wewe Zombie, Moyo na Utu wako wa kwenda kumuona kumepekekea na sie kujua hali ya mwenzetu, InshaAllah Mwenyezi Mungu Amjaalie kupona…”.
Diamond alihimiza pia watu wengine waendelee kumchangia Bacteria akisema kwa sasa anahitaji watu sana.