Chama cha Wahariri wa Habari Nchini (KEG) kimemteua Naibu Mhariri Mkuu wa Shirika la Utangazaji Nchini (KBC) Millicent Awuor kuwa mwenyekiti wake wa kamati ya mipango.
Awuor anachukua wadhifa ulioshikiliwa na Linda Bach, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho.
Mabadiliko hayo yalitangazwa na Rais wa KEG Zubeidah Kananu, kupitia kwa taarifa jana Jumatatu jioni.
Naye Bach ambaye ni mhariri wa zamani katika kampuni ya Standard Group, anachukua nafasi ya Rosalia Omungo ambaye muhula wake umemalizika.
Omungo amehudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa KEG kwa muda wa miaka minane iliyopita.
Kananu alisifu uongozi wa Omungo, akielezea kipindi chake kama cha uongozi kuwa bora huku akimtakia mafanikio katika majukumu yake yajayo.
Uteuzi wa Bach una maanisha atalazimika kujiuzulu kutoka wadhifa wake kama mwanachama wa baraza la uchapishaji la halmashauri kuu ya chama hicho.
Kwa mujibu wa katiba ya chama, baraza hilo limemteua Andy Kagwa wa Standard Group kuchukua nafasi hiyo.