Chama cha Jubilee kimetangaza kuwa kitawasilisha wagombea kwenye nyadhifa zote katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa chama hicho, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye pia ni kiongozi wa Jubilee, amesema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba kila mtu ana haki ya kugombea wadhifa wowote ule anaoutaka.
“Haijalishi ikiwa wewe ni Hasla au uko na pesa, kila mtu ana haki ya kuongoza taifa letu,” alisema Uhuru wakati wa mkutano uliohudhuriwa na Waziri wa zamani wa Usalama wa Taifa Dkt. Fred Matiang’i.
Dkt. Matiang’i ametangaza kuwa atagombea urais na kuna uwezekano mkubwa wa yeye kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2027.
Uhuru akitumia fursa hiyo kuishambulia serikali ya Kenya Kwanza kwa kuanzisha miradi ya majaribio ambayo alisema imeshindwa kuzaa matunda na hivyo kuwafungulia Wakenya mvua ya masaibu.
Kulingana naye, mipango iliyoanzishwa na utawala wake kama vile Linda Mama imeborongwa na utawala wa sasa badala ya kuboreshwa kwa manufaa ya Wakenya.
Badala yake, mipango mingine kama vile Mamlaka ya Afya ya Jamii, SHA imeanzishwa na kuibua changamoto si haba katika sekta ya afya.
Hata hivyo, mkutano wa Jubilee ulisusiwa na viongozi wengine wa upinzani kama vile Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua.
Badala yake, wote hao waliamua kuhudhuria mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa chama cha People’s Liberation Party, PLP, chake Martha Karua uliofanyika katika jumba la Ufungamano jijini Nairobi.