Maafisa wa polisi wametangaza kukamatwa kwa mshukiwa wa pili wa tukio la kuidhalilisha bendera ya Kenya katika uwanja wa michezo wa Nyayo.
Katika taarifa, Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI ilitangaza kutiwa mbaroni kwa Muhidin Ahmed Abukar wa umri wa miaka 14 pekee.
Kukamatwa kwake kulijiri saa chache tu baada ya mwenzake wa umri wa miaka 17 aitwaye Ibrahim Haidar Yusuf na kwa sasa wawili hao wanazuiliwa na polisi wakisubiri hatua zitakazofuata.
Vijana hao wawili wanaoaminika kuwa wa asili ya Somalia walionekana kwenye video iliyosambaa mitandaoni wakiidhalilisha bendera ya Kenya wakati wa mechi ya kandanda katika uwanja wa Nyayo.
Tukio hilo lilitokea Septemba 20, 2025, wakati wa mechi kati ya Mogadishu City Club na Police FC.
Wawili walionekana wakikanyaga, kuipiga teke na kuidhalilisha bendera ya taifa, jambo lililozua hasira na shutuma kutoka kwa umma, mitandaoni na uwanjani.
DCI ilitaja kitendo hicho kuwa kinyume cha sheria na kinavunjia heshima maadili na thamani tunazoziheshimu kama taifa.
Kulingana na Kifungu cha 2B cha Sheria ya Bendera ya Kitaifa, Alama na Majina, Sura ya 99, yeyote anayeonesha dharau kwa bendera ya taifa, wimbo wa taifa au alama zilizobainishwa anatenda kosa la jinai.