Tiwa Savage azungumzia video yake iliyovujishwa

Marion Bosire
2 Min Read
Tiwa Savage

Mwanamuziki na mtunzi wa nyimbo kutoka Nigeria, Tiwatope Savage, maarufu kama Tiwa Savage, amefichua kuwa kanda yake ya ngono iliyovuja mwaka 2021 ilisambazwa kama sehemu ya mchezo wa kamari.

Tiwa alielezea tukio hilo kuwa moja ya nyakati za maumivu makubwa zaidi maishani mwake.Nyota huyo wa muziki wa Afrobeats pia alifichua kuwa amekuwa akiishi bila kushiriki ngono kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Alifichua haya wakati wa mahojiano na kipindi cha The Breakfast Club ambapo alizungumza kwa uwazi kuhusu jinsi kashfa hiyo iliathiri maisha yake binafsi, taaluma yake, na afya yake ya akili.

Savage alisema kuwa awali alikabiliana na hali hiyo kwa kutumia ucheshi na kuelekeza maumivu hayo kwenye nyimbo zake, lakini alikiri kwamba tukio hilo lilimuumiza kwa undani zaidi.

“Nilipozungumza kuhusu ile kanda ya ngono ndivyo nilivyojaribu kuvuka kipindi hicho. Lakini nikitazama nyuma, je, kweli nilikabiliana nayo? Sidhani. Niliumia… nilikuwa mhanga,” alisema.

Alifichua kuwa wakati huo mpenzi wake alidai kuwa kanda hiyo ilivujishwa kimakosa, lakini baadaye aligundua kwamba ilisambazwa kama sehemu ya dau kati yake na marafiki zake.

“Alisema alikuwa anajaribu kuihifadhi, kisha akabonyeza kitufe cha ‘tuma’ kwa bahati mbaya… Baadaye niligundua kuwa ilikuwa dau kati yake na marafiki zake,” alisema.

Mwanamuziki huyo aliongeza kuwa watu wengi walidhani kuwa alichochea uvujaji huo makusudi ili kujiongezea umaarufu.

Share This Article