Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) imekumbwa na ukosoaji mkali kutoka kwa wabunge kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya kikatiba kuhusu utofauti na ujumuishaji katika ajira zake.
Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Mshikamano na Fursa Sawa, Mkurugenzi Mkuu wa AFA, Bruno Linyiri, alikiri kuwa Mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi bila mwongozo wa rasilimali watu tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2013.
Jambo hilo limezuia utekelezaji wa sheria kuhusu usawa wa kikabila na uwakilishi wa makundi maalum katika ajira.
“Mamlaka haijawahi kuwa na mwongozo wa rasilimali watu tangu ilipoanzishwa. Wafanyakazi wetu waliteuliwa tu. Hatujawahi kuajiri moja kwa moja. Hata hivyo, mwaka huu tumepokea mfumo wa HR unaohitajika na tunapanga kuajiri huku tukishughulikia dosari zilizobainishwa na Mkaguzi Mkuu,” alielezea Linyiri.
Kikao hicho kilichoongozwa na Duncan Mathenge mbunge wa Nyeri mjini, kilieleza wasiwasi kuhusu ukosefu wa usawa wa kikabila ndani ya Mamlaka hiyo, ambapo jamii mbili zinaripotiwa kutawala idadi ya wafanyakazi kwa asilimia 94 na 84 mtawalia.
“Hili halikubaliki. AFA haionyeshi sura ya Kenya,” Mathenge alisema.
Wajumbe wa Kamati pia waliishutumu AFA kwa kubagua walemavu katika ajira na upatikanaji wa fursa.
Mbunge wa Kamukunji Yusuf Hassan alieleza kuwa rekodi ya AFA ni “ukiukaji wa mara kwa mara wa Katiba”, na akauliza kwa nini walemavu wengi huajiriwa kama wafanyakazi wa muda tu.
“Hoja yako kwamba ukosefu wa uzoefu unawazuia walemavu ni ya kibaguzi. Watawezaje kupata uzoefu ikiwa hawapewi fursa?” alihoji.
Mbunge wa Narok Kaskazini Agnes Pareyio na Liza Chelule wa Kaunti ya Nakuru waliihimiza AFA kushirikiana na wabunge kubaini walemavu waliostahiki katika maeneo bunge yao, wakisema kuwa data ipo kwenye ngazi ya mashinani.
Wabunge wengine, akiwemo Joshua Oron wa Kisumu ya Kati, Martin Owino wa Ndhiwa na Dick Maungu wa Luanda walisema kuwa kukosekana kwa mwongozo wa rasilimali watu kumeacha mianya kwa usimamizi kukwepa sheria za ajira.
Kando na masuala ya ajira, wabunge waliitaka AFA kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi yaliyotengwa kwa kusaidia upatikanaji wao wa mikopo.
Mbunge mteule Denar Hamisi aliitaka Mamlaka kuwa wadhamini wa makundi maalum yanayotafuta mikopo kutoka kwa benki za kibiashara, kama inavyofanywa na mashirika mengine ya serikali.
Mathenge aliagiza AFA kuhakikisha kuwa zoezi lake lijalo la uajiri linashughulikia ukosefu wa usawa wa kikabila na kukuza uwakilishi wa haki wa wanawake, vijana na PLWDs.
“Hii ni nafasi yenu kurekebisha dosari hizi na kuzingatia kanuni ya kikatiba ya ujumuishaji,” alimwambia Linyiri.