Mwanamuziki na mwanasiasa wa Uganda Hajat Stecia Mayanja amejipata matatani baada yake kuhudhuria hafla ya chama tawala nchini humo NRM.
Mwimbaji huyo ameitwa na Chama cha National Peasants’ Party – NPP, kufuatia uhusika wake katika mkutano huo wa kisiasa wa NRM uliofanyika Kololo.
Katika tangazo kwa umma lililotolewa na Katibu Mkuu wa chama, Stecia ameagizwa kufika mbele ya Kamati Kuu ya Utendaji ya Kitaifa (NEC) leo, Septemba 25, 2025, saa 10:00 jioni katika makao makuu ya chama.
Kulingana na taarifa hiyo, Stecia anakabiliwa na tuhuma za kushiriki mikutano ya kisiasa ya NRM, jambo linalochukuliwa kuwa kinyume na Katiba ya Chama cha NPP.
“Chama cha NPP, kupitia Katibu Mkuu, kinamwita rasmi Hajat Stecia Mayanja Faridah kufika mbele ya Kamati Kuu ya Utendaji ya Kitaifa (NEC) tarehe 25 Septemba 2025, saa 10:00 jioni katika Makao Makuu ya Chama” ilisema taarifa hiyo.
Iliendelea kuelezea kwamba anahitajika kujibu tuhuma hizi na atapewa fursa ya kusikilizwa kwa haki. Iwapo atashindwa kufika bila sababu ya msingi anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Stecia, ambaye pia ni Rais wa Chama cha NPP, bado hajatoa tamko lolote kuhusu wito huo.