Bunge laidhinisha uteuzi wa mabalozi 9

Marion Bosire
2 Min Read
Florence Bore akiapishwa kabla ya usaili bungeni

Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa watu tisa walioteuliwa kuhudumu kama Makamishna Wakuu, Mabalozi na Mawakala Wakuu wa Balozi.

Uamuzi huo umetolewa kufuatia kupitishwa kwa Ripoti kutoka kwa Kamati ya Kisekta ya Ulinzi, Ujasusi na Masuala ya Kigeni, ambayo ilipendekeza kuidhinishwa kwa wawania wote baada ya kuwapiga msasa mkali mapema mwezi huu.

Kamati hiyo ilibaini kuwa wawania hao wana sifa stahiki za kitaaluma, uwezo wa kitaaluma na uadilifu wa kibinafsi unaohitajika ili kuwakilisha vyema taifa la Kenya katika jukwaa la kimataifa.

Walioteuliwa ni pamoja na Florence Chepngetich Bore atakayehudumu kama kamishna mkuu wa Kenya huko Windhoek, Namibia, Anthony Mwaniki Muchiri atakayehudumu kama balozi wa Kenya jijini Ankara, nchini Uturuki na Lucy Kiruthu atakayekuwa balozi wa Kenya huko Bangkok nchini Thailand.

Wengine ni Henry Wambuma atakayekuwa Balozi wa Kenya jijini Bujumbura nchini Burundi, Abdirashid Salat Abdille ameteuliwa kuwa balozi wa Kenya jijini Jakarta nchini Indonesia na Joseph Musyoka Masila balozi wa Kenya jijini Riyadh nchini Saudi Arabia.

Wanaofunga orodha hiyo ni Edwin Afande balozi wa Kenya huko Vienna, Austria, Jayne Jepkorir Toroitich aliyeteuliwa kuwa wakala mkuu wa balozi huko Dubai, katika Falme za Kiarabu na Judy Kiaria Nkumiri wakala mkuu wa Balozi, jijini Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Share This Article