Bobi Wine asema hii ni awamu ya mwisho ya ukombozi wa Uganda

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki ambaye pia ni mwanasiasa nchini Uganda Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine amesema kwamba hii ndiyo zamu ya mwisho ya mapambano ya kukomboa taifa la Uganda.

Alisema haya muda mfupi tu baada ya kuidhinishwa rasmi kuwania Urais wa taifa hilo la Afrika mashariki leo.

Akihutubia wafuasi wake katika uwanja wa tume ya uchaguzi ya Uganda huku mvua kubwa ikinyesha, Bobi Wine alisema, ni awamu ya mwisho ya mapambano ya kukomboa Uganda kutokana na miongo kadhaa ya uongozi mbaya na ukandamizaji.

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha National Unity Platform – NUP aliteuliwa na tume ya uchaguzi ya Uganda leo kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026 na hivyo kufunga mchakato wa uteuzi.

Wine sasa amejiunga na wawaniaji wengine watano wa Urais akiwemo Rais Yoweri Museveni anayetafuta muhula mwingine mamlakani baada ya kuongoza nchi hiyo kwa miaka 39.

Msanii huyo alipatiwa nakala ya sajili ya kitaifa ya wapiga kura na ulinzi wa serikali na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Uganda Simon Byabakama.

Kulingana na Bobi, uteuzi wake leo sio tu kibali cha kuanza kampeni bali pia ni malalamiko kuhusu ukosefu wa haki ambao raia wa Uganda wamevumilia kwa zaidi ya miongo minne.

Bobi Wine alishukuru watu wa Uganda kwa kuendelea kumwamini tangu alipowania Urais kwa mara ya kwanza mwaka 2021, akisema moyo wake umejaa hisia za uwajibikaji ili kuhakikisha anatekeleza ahadi yake ya Uganda mpya.

Share This Article