Rais wa Malawi Dkt. Lazarus Chakwera amekiri kushindwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo Septemba 16 mwaka huu.
Kwenye hotuba kwa taifa leo Jumatano, Dkt. Chakwera amewashukuru raia wa nchi hiyo kwa kumpa fursa ya kuhudumu kama rais wa sita wa nchi hiyo.
Ameahidi kukabidhi madaraka kwa amani kwa mrithi wake, Rais wa zamani Prof. Peter Mutharika.
Dkt. Chakwera, mwenye umri wa miaka 70, amewataka raia wa nchi hiyo kuunga mkono utawala mpya wa nchi hiyo.
Tume ya Uchaguzi nchini humo (MEC) inatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo majira ya saa tisa alasiri leo Jumatano.
Hatua ya Dkt. Chakwera kukiri kushindwa ina maana kwamba Prof. Mutharika anatarajiwa kutangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa urais nchini humo.
Prof. Mutharika aliye na umri wa miaka 85, anaongoza kwa karibu asilimia 66 ya kura zote zilizohesabiwa kufikia sasa na tume ya uchaguzi nchini Malawi.
Matokeo hayo yanaashiria kurejea mamlakani kwa Mutharika aliyetimuliwa kwenye wadhifa huo miaka mitano iliyopita baada ya kushindwa na Chakwera kwenye uchaguzi mkuu.
Kulingana na tume ya uchaguzi, mshindi wa kinyang’anyiro hicho ni sharti apate asilimia 50 na kura moja kati ya kura zote zilizopigwa.
Inaaminika Chakwera amepoteza umaarufu kutokana na kutotimiza ahadi zake za kabla ya uchaguzi, ikiwemo kufufua uchumi wa nchi hiyo.