Hongo ya shilingi elfu 10 imemweka msajili wa ardhi katika kaunti ya Busia matatani.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inasema ilimkamata Collins Aiela Liyayi jana Jumanne alasiri kwa kuitisha hongo ya shilingi elfu 10 kutoka kwa mlalamikaji.
Afisa huyo alikamatwa katika operesheni iliyoendeshwa na afisi ya kanda ya magharibi ya tume hiyo.
Kulingana na EACC, msajili huyo aliitisha hongo kutoka kwa mlalamikaji kama sharti la kumkabidhi hatimiliki ya ardhi ambayo alikuwa ameitayarisha ila akakataa kuipeana hadi “ada ya kuitoa” ilipwe.
Ni hongo ambayo aliipokea ila hakufahamu mienendo yake ilifuatiliwa kwa karibu na maafisa wa upelelezi.
Tume inasema afisa huyo alimakamatwa katika operesheni iliyofuatia malalamishi chungu nzima kuwa Liyayi amekuwa na hulka ya kuitisha hongo kutoka kwa wakazi wa Busia kabla ya kuwakabidhi hatimiliki zao za ardhi.
Mshukiwa alipelekwa hadi afisi ya EACC ya kanda ya magharibi mjini Bungoma alikoandikisha taarifa na kisha kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma akisuburi kuandikisha taarifa zaidi leo Jumatano na kisha kufikishwa mahakamani.
EACC imeimarisha msako dhidi ya ulaji rushwa katika utumishi wa umma kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa raia.