Ubabe wa kisiasa kati ya Gavana wa sasa wa Kakamega Fernandes Barasa na mtangulizi wake Wycliffe Oparanya unaonekana kuongezeka huku viongozi hao wawili wakizidi kurushiana cheche kali za maneno.
Katika malumbano ya hivi punde, Barasa ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kakamega amemtaka Oparanya kukoma kumdunisha mbele ya wakazi wa kaunti hiyo.
Akiwahutubia wanahabari katika eneo bunge la Malava, Gavana Barasa alimshutumu Oparanya ambaye pia ni Waziri wa Vyama vya Ushirika kwa kudunisha uongozi wake mara kwa mara hadharani na kumtaka akome tabia hiyo.
Awali, Oparanya alimshutumu Barasa akimtuhumu kwa kupanga njama ya kumharibia sifa kisiasa na kuahidi kuzikabili njama hizo kwa nguvu sawia.
Ni shutuma ambazo zimepuuziliwa mbali na Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula akizitaja kuwa zisizokuwa na msingi.
Kulingana na Savula, uongozi wa sasa wa kaunti hiyo hauna kusudi la kumdunisha Oparanya.
Aliongeza kuwa Mamlaka ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) iliomba faili fulani kuhusiana na uchunguzi wa ufisadi unaoendelea dhidi ya Gavana huyo wa zamani.
Oparanya anaona mkono wa Barasa kwenye masaibu yanayomkumba ambapo kesi ya ufisadi dhidi yake imefufuliwa.
Kulingana na Waziri huyo wa Vyama vya Ushirika, Barasa ameibuka kuwa msaliti licha ya kumsaidia kumrithi kama Gavana wa kaunti ya Kakamega katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.