Pigo kwa Lissu baada ya mahakama kutupilia mbali maombi yake

Dismas Otuke
1 Min Read

Juhudi za kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA, Tundu Lissu, kuondolewa mashtaka ya makosa ya uhaini zimeambulia pakavu baada ya mahakama kutupilia mbali maombi ya mwanasiasa huyo.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani alikuwa ameitaka mahakama ifute makosa yote ya uhaini kwa kusema hakuna ushahidi wa kutosha.

Lissu alinukuliwa mwezi Aprili mwaka huu akiwachochea Watanzania kuzuia kuandaliwa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kuandaliwa mwezi ujao.

Hata hivyo, akitoa uamuzi leo Jumatatu, Jaji Danstan Ndunguru amethibitisha kuwa makosa yote ya kesi za jinai dhidi ya Lissu yanapaswa kuendelea mbele na pia yana ushahidi wa kutosha.

Aidha, Lissu amekubali kutoa matamshi hayo, ila akasema sio ya uhaini bali ni ya kisiasa tu.

Endapo atahukumiwa kifungo cha maisha gerezani ambayo ni adhabu ya kesi ya jinai, utakuwa mwisho wa amali ya siasa kwa Lissu ambaye pia ni wakili.

 

Share This Article