Hamna haja ya wakazi wa Mandera kuhofia usalama wao kutokana na visa vya hivi karibuni kwenye mpaka wa Kenya na Somalia.
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen amewahakikishia wakazi hao kwamba serikali ya Kenya Kwanza imedhamiria kulinda raia wote na kudumisha sheria katika eneo hilo.
Akizungumza wakati wa kongamano la Jukwaa la Usalama lililoandaliwa katika kaunti ya Mandera leo Jumatatu, Murkomen aliahidi kuwa Kenya italinda uadilifu wa mipaka yake na Somalia bila kuhatarisha maisha ya mtu yeyote.
“Tunataka kuwahakikishia watu wa Mandera na eneo lote la Kaskazini Mashariki kuwa usalama wao ni kipaumbele chetu,” aliahidi Waziri huyo ambaye amekuwa akiongoza makongamano ya Jukwaa la Usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi, hili lilikiwa la 44.
Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi kusalia watulivu na kushirikiana na asasi za usalama kufanikisha azima ya serikali ya kuwalinda.
Aidha, aliwataka kupiga ripoti kwa maafisa wa usalama kuhusiana na shughuli zozote wanazozitilia shaka.
Moja ya malengo ya makongamano ya Jukwaa la Usalama ni kukuza uhusiano wa karibu na serikali za kaunti na maafisa wa usalama katika maeneo ya vijijini.
