Chama cha Wanasheria nchini, LSK kimemteua wakili wa kuiwakilisha familia huku uchunguzi ukiendelea kubaini namna kifo cha Simon Warui kilivyotokea wakati akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Mombasa.
Warui ameripotiwa kukumbana na mauti jana Jumapili, majira ya saa nne asubuhi.
“LSK inafuatilia kisa cha Bw. Simon Warui aliyefariki wakati akizuiliwa katika kituo cha polisi cha Central, Mombasa. Tumemteua wakili wa kuiwakilisha familia katika kufuatilia uchunguzi unaoendelea na kuhakikisha ukweli kamili na hali iliyosababisha kifo cha Bw. Warui vinawekwa wazi, na mtu aliyehuika kuwajibishwa,” amesema Rais wa LSK Faith Odhiambo kwenye taarifsa.
“Tumepokea ripoti kutoka kwa familia zinazoashiria kwamba alitoweka majira ya saa nne asubuhi siku ya Jumapili na ripoti kupigwa katika kituo cha polisi cha Embakasi. Hali iliyosababisha kifo chake katika kituo cha polisi cha Mombasa bado haijulikani, lakini tunafanya kazi kwa karibu na washirika wa mashirika ya kijamii na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu KNCHR kuhakikisha suala hilo linachunguzwa haraka na kuhitimishwa.”
Kifo cha Warui kinatokea takriban miezi miezi minne tu baada ya kile cha Albert Ojwang kutokea katika kituo cha polisi cha Central jijini Nairobi.
Mamlaka ya Kuangazia Utendakazi wa Polis, IPOA, imekuwa ikifanya uchunguzi wa kubaini waliomuua Ojwang na hadi hii leo, haijatoa ripoti kamili kuhusu namna mauaji ya Ojwang yalivyotokea.