Kenya na Cyprus zinatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano, huku zikiweka msingi wa makubaliano ya mkakati wa kina utakaoongoza ushirikiano katika sekta mbalimbali za uchumi.
Waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi alisema kufuatia mkataba wa makubaliano ulioafikiwa mwezi Julai kuhusu mashauriano ya kisiasa, nchi hizo mbili zilitia saini mkataba wa kilimo.
Mkataba huo unazingatia zaidi kilimo bora, uendelevu, uvumbuzi na msaada kwa wakulima.Ushirikiano huo pia utahusu mafunzo ya polisi, Jumuiya ya Madola na umoja wa mataifa.
Mudavadi alisema haya baada ya kufanya mkutano na waziri wa mambo ya nje wa Cyprus Constantinos Kombos. Wawili hao walikutana pembezoni mwa mkutano mkuu wa 80 wa Umoja wa Mataifa mjini New York, nchini Marekani.
Wakati huo huo, Mudavadi alitangaza ziara ya kihistoria ya kwanza kabisa ya Rais Nikos Christodoulides wa Cyprus nchini Kenya.
Alisema ziara hiyo itaweka mazingira ya kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili na kuinua uhusiano huo katika ngazi mpya ya kimkakati.
Miongoni mwa maeneo kipaumbele ni pamoja na elimu, utalii, masuala ya bahari, na nishati mbadala.